Daniel 5

Maandishi Ukutani

1 aMfalme Belshaza alifanya karamu kubwa kwa ajili ya maelfu ya wakuu wake na akanywa mvinyo pamoja nao. 2 bWakati Belshaza alipokuwa akinywa mvinyo wake, aliamuru viletwe vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekaluni huko Yerusalemu, ili mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake waweze kuvinywea. 3Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka Hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake wakavinywea. 4 cWalipokuwa wakinywa mvinyo, wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, ya shaba, chuma, miti na mawe.

5Ghafula vidole vya mkono wa mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika. 6 dUso wa mfalme ukageuka rangi, naye akaogopa sana, kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea.

7 eMfalme akawaita wasihiri, wanajimu na waganga waletwe, naye akawaambia hawa wenye hekima wa Babeli, “Yeyote asomaye maandishi haya na kuniambia maana yake atavikwa nguo za zambarau, na kuvikwa mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atafanywa mtawala wa cheo cha tatu katika ufalme.”

8 fNdipo watu wote wa mfalme wenye hekima wakaingia, lakini hawakuweza kusoma yale maandishi wala kumwambia mfalme maana yake. 9 gBasi Mfalme Belshaza akazidi kujawa na hofu, na uso wake ukageuka rangi zaidi. Wakuu wake wakapigwa na bumbuazi.

10 hMalkia
Au: Mama yake mfalme.
aliposikia sauti za mfalme na wakuu wake, alikuja katika ukumbi wa karamu. Akasema, “Ee mfalme, uishi milele! Usishtuke! Usibadilike rangi kiasi hicho!
11 jYuko mtu katika ufalme wako ambaye ana roho ya miungu mitakatifu ndani yake. Wakati wa baba yako, mtu huyo alionekana kuwa na ufahamu, akili na hekima kama ile ya miungu. Mfalme Nebukadneza baba yako, yaani nasema mfalme baba yako, alimweka kuwa mkuu wa waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi. 12 kMtu huyu Danieli, ambaye mfalme alimwita Belteshaza, alionekana kuwa na akili nyepesi, maarifa na ufahamu, pia uwezo wa kufasiri ndoto, kueleza mafumbo na kutatua matatizo magumu. Mwite Danieli, naye atakuambia maana ya haya maandishi.”

13 lHivyo Danieli akaletwa mbele ya mfalme, naye mfalme akamuuliza, “Je, wewe ndiwe Danieli, mmoja wa watu wa uhamisho walioletwa na mfalme baba yangu kutoka Yuda? 14Nimesikia kwamba roho ya miungu iko ndani yako, na kwamba una ufahamu, akili na hekima ya pekee. 15 mWatu wenye hekima na wasihiri waliletwa mbele yangu ili kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, lakini hawakuweza kunifafanulia. 16 nBasi nimesikia kwamba unaweza kutoa tafsiri na kutatua matatizo magumu. Ikiwa unaweza kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, utavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utafanywa mtawala wa tatu katika ufalme.”

17 oNdipo Danieli akamjibu mfalme, “Waweza kubaki na zawadi zako mwenyewe na kumpa mtu mwingine zawadi zako. Hata hivyo, nitasoma maandishi kwa mfalme na kumwambia maana yake.

18 p“Ee mfalme, Mungu Aliye Juu Sana alimpa baba yako Nebukadneza utawala, ukuu, utukufu na fahari. 19 qKwa sababu ya nafasi ya juu aliyompa baba yako, kabila zote za watu, mataifa na watu wa kila lugha walimhofu na kumwogopa. Wale ambao mfalme alitaka kuwaua, aliwaua; wale aliotaka kuwaacha hai, aliwaacha hai; wale aliotaka kuwapandisha cheo, aliwapandisha; aliotaka kuwashusha, aliwashusha. 20 rLakini moyo wake ulipokuwa na majivuno na kuwa mgumu kwa kiburi, aliondolewa kutoka kwa kiti chake cha ufalme na kuvuliwa utukufu wake. 21 sAkafukuzwa mbali na wanadamu na kupewa akili ya mnyama, akaishi pamoja na punda-mwitu, akala majani kama ng’ombe, nao mwili wake ukaloweshwa kwa umande wa mbingu, mpaka alipotambua kwamba Mungu Aliye Juu Sana ndiye mtawala juu ya falme za wanadamu na kwamba humtawaza juu yao yeyote amtakaye.

22 t“Lakini wewe mwanawe, ee Belshaza, hukujinyenyekeza, ingawa ulifahamu haya yote. 23 uBadala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea mvinyo. Ukaisifu miungu ya fedha na dhahabu, ya shaba, chuma, miti na mawe, miungu ambayo haiwezi kuona, au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake. 24Kwa hiyo ameutuma mkono ule ulioandika maneno.

25“Haya ndiyo maneno yaliyoandikwa: mene, mene, tekeli na peresi

26 v“Hii ndiyo maana ya maneno haya: Mene: Mungu amezihesabu siku za utawala wako na kuukomesha.
27 w Tekeli: Wewe umepimwa katika mizani na umeonekana umepungua.

28 x Peresi: Ufalme wako umegawanywa na kupewa Wamedi na Waajemi.”

29 yNdipo kwa amri ya Belshaza, Danieli akavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni, tena akatangazwa kuwa mtawala wa tatu katika ufalme.

30 zUsiku ule ule, Belshaza mfalme wa Wakaldayo akauawa, 31 aanaye Dario Mmedi akashika ufalme akiwa na miaka sitini na miwili.
Copyright information for SwhKC